Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Musawi—Imamu wa Ijumaa wa Baghdad na mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Hawza ya Najaf Ashraf—katika khutba za Ijumaa alitoa uchambuzi mpana wa hali ya kisiasa nchini Iraq na matukio ya eneo. Katika hotuba yake, alizungumzia matokeo ya uchaguzi wa bunge, mipango ya Marekani na utawala wa Kizayuni katika Mashariki ya Kati, na matukio ya hivi karibuni nchini Lebanon baada ya shahada ya Sayyid Hassan Nasrallah.
Katika sehemu ya kwanza ya khutba, Ayatullah Musawi alisisitiza kuwa; matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni ni ujumbe wa wazi kuhusu uelewa na weledi wa wananchi wa Iraq. Alisema kuwa mitazamo inayojitambulisha kama “ya kiraia” na inayoungwa mkono na Marekani, licha ya kuwa na takribani wagombea 400, imepata kiti kimoja tu. Kwa mujibu wake, kundi hili lilikuwa likijaribu, kupitia kaulimbiu ya uhuru, kubadilisha utambulisho wa kidini wa bunge na kudhoofisha thamani za kijamii, lakini umakini wa wananchi umeangusha mradi huu na kwa mara nyingine kuthibitisha utambulisho huru wa Iraq.
Imamu wa Ijumaa Baghdad aliendelea kusema kuwa; idadi ya wawakilishi wa Kishia katika bunge jipya imefikia 197, na kwamba kwa mara ya kwanza uwezekano wa kuchagua nguzo zote tatu kuu za serikali kutoka “nyumba ya Kishia” umejitokeza. Hata hivyo, alisisitiza kuwa shinikizo la Marekani bado linazuia kuundwa kwa demokrasia halisi inayotokana na kura ya wengi.
Ayatullah Musawi pia alivitaka vyama vya kisiasa kuweka vigezo vya wazi katika kumchagua waziri mkuu ajaye: waziri mkuu aliye mchamungu, mwenye uwezo, anayesimama imara mbele ya vishawishi vya madaraka na pesa, na mwenye mpango wa marekebisho unaotekelezeka kwa ajili ya kuendesha nchi.
Katika sehemu ya hotuba inayohusu eneo, Imamu wa Ijumaa Baghdad aliangazia kuwa matukio ya Ghaza na Lebanon ni sehemu ya mpango wa Marekani–Israel wa kutengeneza upya ramani ya Mashariki ya Kati; mpango ambao kwa mujibu wake unalenga kuthibitisha nafasi ya utawala wa Kizayuni kama mhimili wa kiusalama na kisiasa wa eneo. Aliutaja mpango uliowasilishwa katika Baraza la Usalama kwa jina la “Amani kwa Ghaza” kuwa ni mfumo mpya wa kugawa upya ushawishi na kuchora mipaka ya kisiasa ya eneo, na akaongeza kuwa kuna juhudi pia za kuivuta Iraq kuingia kwenye mhimili huo.
Pia alizungumzia uwepo wa siri wa waziri mkuu wa Iraq, ambaye muda wake unakaribia kuisha, katika mkutano wa Sharm el-Sheikh, na kusisitiza kuwa hatua hiyo ilikuwa yenye lengo la kuweka mazingira ya mchakato wa uhusiano wa kawaida na kurefusha kipindi chake cha uongozi, lakini upinzani na ueledi wa wananchi umeufanya mpango huo ushindwe.
Katika sehemu iliyohusu Lebanon, Ayatullah Musawi alisema kuwa; shahada ya Sayyid Hassan Nasrallah na makamanda wa muqawama, kinyume na propaganda za maadui, haijapunguza nguvu ya muqawama bali imezidi kuonesha uimara na mshikamano wake. Alisema kuwa utawala wa Kizayuni katika wiki za karibuni umekuwa ukijaribu kubadilisha mizania nchini Lebanon kupitia ugaidi na mashambulizi ya anga, lakini haujapata mafanikio yoyote ya kisiasa au kijeshi.
Aliongeza kuwa madai ya kuanguka kwa muqawama ni “ya kipuuzi na yasiyo na msingi,” na akakumbusha kuwa baadhi ya kauli zilizotolewa ndani ya Lebanon katika mwelekeo huo, zilirejeshwa mara moja.
Ayatullah Musawi alihitimisha kwa kusisitiza kuwa siku zijazo zitaonesha wazi kushindwa kwa kamari ya Israel, na akasema: “Jibu lipo njiani… na kesho iko karibu zaidi kuliko inavyodhaniwa.”
Maoni yako